Kufanya Kazi nchini Ufini

Mradi wa Mafunzo ya Kutangamana kwa Wahamiaji

Unapohamia katika manispaa yako, jisajili katika ...

Kutafuta Ajira

Kutafuta ajira nchini Ufini huhitaji kujituma na kuwa na ukaribu na watu, ingawa wahamiaji husaidiwa katika mchakato wa kutafuta ajira. Ofisi za TE hutoa ...

Wajibu na Haki za Wafanyakazi

Mfanyakazi hufanya kazi saa 40 kwa wiki na saa 8 kila siku. Hata hivyo, idadi ya saa kamili hutegemea taaluma ya ...

Utamaduni wa Kazi nchini Ufini

Ikilinganishwa na nchi nyingine utamaduni wa nchi ya Ufini una aina ya usawa wa kipekee. Wafanyakazi na waajiri huitana ...




Kuelekea Maisha ya Kufanya Kazi

Kumbuka kwamba lugha inayotumika katika mazingira ya kazi nchini Ufini ni Kifini. Sehemu za kazi ambazo lugha ya kazi ni Kiingereza ni chache sana. Ni lazima ujifunze lugha ya Kifini ndipo uajiriwe nchini Ufini.

Mradi wa Mafunzo ya Kutangamana kwa Wahamiaji

Unapohamia katika manispaa yako, jisajili katika Ofiisi yako ya Ajira na Maendeleo ya Uchumi (ofisi ya TE) kama mtu anayetafuta kazi. Maafisa katika ofisi hiyo watakusaidia kuhusu masuala yanayohusu ajira na mafunzo ya kazi, na utapata taarifa kuhusu nafasi za kazi. Wewe kama mhamiaji una haki za kupata huduma sawa na wananchi wa Ufini.

Kama mhamiaji halali una haki ya kuwekwa kwenye mpango wa kutanganama kwa miaka ya kwanza mitatu katika makazi yako nchini Ufini. Mpango wa kutangamana utaundwa kati yako, afisa wa ustawi wa jamii na afisa kutoka ofisi ya TE katika manispaa yako. Kwanza, tathmini ya awali itafanywa kuhusu elimu yako, uzoefu wa kazi ulionao na ujuzi wako wa lugha. Kwa hivyo ni muhimu kubeba vyeti vyako vya elimu na stakabadhi za kazi unapohudhuria tathmini hii, na uwe na orodha ya kazi zote ambazo umewahi kufanya.

Wewe na familia yako mtaundiwa mkakati wa kutangamana kutokana na matokeo ya tathmini ya awali. Mpango huu utajumuisha mafunzo ya lugha ya Kifini, mafunzo ya maandalizi ya kazi, na mafunzo ya ufundi. Mpango wa watoto na vijana kuhusu maandalizi yao kwa ajili ya elimu ya msingi utazingatiwa. Wahamiaji wote lazima washiriki katika mpango wa kutangamana, kadhalika kushiriki katika shughuli walizokubaliana katika mpango wa kutangamana. Kwa kawaida mpango wa kutangamana huwa ni wa mwaka mmoja.

Wahamiaji watu wazima huanza mpango wa kutangamana na masomo ya mafunzo yanayolenga kujifunza lugha ya Kifini. Watoto na vijana huanza maandalizi yao ya shule wanapofika shule ya msingi, na baadaye, huendelea na masomo yao ya elimu ya kawaida ya shule za msingi. Kama kuna mtoto mdogo nyumbani, mama yake anaweza kupewa mpango rahisi wa kutangamana.

Kutafuta Ajira

Kutafuta ajira nchini Ufini huhitaji kujituma na kuwa na ukaribu na watu, ingawa wahamiaji husaidiwa katika mchakato wa kutafuta ajira. Ofisi za TE hutoa taarifa kuhusu nafasi za kazi zinazofaa kwa mhamiaji na hutoa usaidizi kwa kuandaa barua za maombi ya kutafuta ajira ziwe tayari wakati wa mafunzo ya kutangamana.

Ni muhimu kuwa na Wasifukazi (CV) na ujifunze namna ya kutafuta kazi mtandaoni, k.m. kupitia kurasa za Wizara ya Ajira na Uchumi. Ni muhimu pia kuandika mifano ya barua ya maombi ya kazi katika lugha ya Kifini na zihaririwe.

Tathmini kuhusu ujuzi ulionao, maarifa yako na kazi ambayo ungependa kufanya. Kupata kazi nchini Ufini, ni fursa ya kuwa na marafiki, wafanyakazi wenzako wapya na fursa za ziada za kuimarisha ujuzi wako wa lugha ya Kifini. Aidha utapata kazi za changamoto mpya, maudhui mazuri na hali ya maisha mpya kabisa. Sehemu nyingi za kazi huwa na huduma za afya na michezo kwa wafanyakazi wao. Ni vizuri kukubali kazi hata kama haioani na ujuzi wako.

Ni nafasi chache sana za kazi hutangazwa kwenye mitandao nchini Ufini. Ndio maana ni muhimu kuwa na ukaribu na marafiki na unaowajua ndio njia mwafaka ya kupata taarifa kuhusu nafasi za kazi. Siku hizi maombi ya kazi nyingi hutumwa mtandaoni, ambayo inahitaji ujuzi wa kutosha na kujua lugha ya Kifini.

Wajibu na Haki za Wafanyakazi

Mfanyakazi hufanya kazi saa 40 kwa wiki na saa 8 kila siku. Hata hivyo, idadi ya saa kamili hutegemea taaluma ya mfanyakazi. Inaruhusiwa kufanya kazi muda wa ziada baada ya kukubaliana na mwajiri. Uko huru kujiunga au kutojiunga na mashirika ya wafanyakazi katika taaluma mahsusi nchini Ufini. Mashirika hutoa ushauri wa kisheria kwa wanachama wao kukiwa na mgogoro, aidha husaidia katika masuala yanayohusu hali za kazi na kufanya kazi.

Unapoanza kazi mpya, mfanyakazi hutia sahihi mkataba na mwajiri wa majukumu yake ya kazi, maslahi ya kazi na malipo waliokubaliana. Mkataba unaweza kuwa wa kudumu au wa kipindi fulani. Mwajiri ana wajibu wa kutoa huduma za afya kwa mfanyakazi na kulipia malipo ya uzeeni ya mfanyakazi.

Mfanyakazi hulipa kodi kwa kazi anayofanya. Ni lazima umpe mwajiri wako kadi ya kutoza kodi, ambayo inaonyesha kodi ya kutoza kutoka kwa mshahara wako. Unaweza kupata kadi ya kutoza kodi kutoka kwenye ofisi ya malipo ya kodi kwenye tovuti ya ofisi ya kodi.

Lazima umwambie mwajiri wako iwapo hujaridhishwa na maslahi yako kazini. Ukihisi kwamba malalamiko yako hayazingatiwi, unaweza kuomba kuonana na msimamizi wa kazini au mwakilishi wa usalama ili uzungumze na meneja. Matatizo yanayohusu kazi yanaweza kujadilliwa na muuguzi au daktari wa sehemu ya kazi.

Udhalimu, ubaguzi au kumbughudhi mtu kwa namna ya kumtaka mapenzi hairuhusiwi kazini nchini Ufini. Ukihisi kuna mtu anayekubughudhi, piga ripoti kwa meneja au daktari wa eneo lako la kazi mara moja.

Mara nyingi ajira huwa ni za mikataba, lakini hata nchini Ufini kuna ajira za ”uchumi wa soko jeusi” ambazo hazina mikataba wala hazilipi kodi. Mhamiaji anashauriwa kuepuka ajira kama hizi. Kazi za siri ambazo hazilipi kodi ni marufuku nchini Ufini, na kazi kama hizi mfanyakazi halindwi na sheria iwapo kutakuwa na tatizo. Kazi ambazo zinakubalika kisheria ambazo kodi haitozwi nchini Ufini ni kuchuma matunda ya forosadi na kuokota chupa pekee.

Ni muhimu kukumbuka kwamba elimu ya ufundi au taaluma fulani na uwezo wa kuzunguma lugha ya Kifini kwa ufasaha kutaimarisha nafasi yako katika masoko rasmi ya kazi.

Utamaduni wa Kazi nchini Ufini

Ikilinganishwa na nchi nyingine utamaduni wa nchi ya Ufini una aina ya usawa wa kipekee. Wafanyakazi na waajiri huitana kwa majina yao ya kwanza. Mara nyingi waajiri hawawasimamii wanyakazi wanapotekeleza majukumu yao. Badala yake, wafanyakazi hupewa majukumu na hutarajiwa kuyatekeleza bila ya usimamizi wowote. Iwapo mfanyakazi hawezi au hajui jinsi ya kutekeleza kazi aliyopewa, anapaswa kuenda moja kwa moja kwa mwajiri ili ampe maelekezo. Katika utamaduni wa kazi nchini Ufini, ni muhimu kuzingatia maelekezo unayopewa kazini.

Ni muhimu pia kuzingatia makataa nchini Ufini. Kimsingi mtu huingia kazini muda aliopangiwa. Ikiwa muda uliopangiwa ni saa 2 asubuhi hufai kuchelewa hata dakika. Kuchelewa huchukuliwa ni kukosa adabu kwa sababu wengine hulazimika kumsubiri aliyechelewa Katika utamaduni wa Ufini ni muhimu kutoa taarifa mapema iwapo unajua kwamba utachelewa. Kama saa zako za kazi si saa maalum za siku, hakikisha unazingatia idadi ya saa za kazi ulizowekewa.

Wafini hujadili masuala yanayohusu kazi moja kwa moja kazini, na hili halichukuliwi kuwa ni utovu wa nidhamu. Kwa mfano, mfanyakazi akigundua kwamba hatapata muda wa kutosha kumaliza kazi fulani, mwajiri anapaswa kuarifiwa moja kwa moja. Wakati wa vikao na mikutano, baada ya salamu washiriki huanza kujadili ajenda za siku mara moja. Mwajiri hatawauliza wafanyakazi wanaendelea vipi. Kwa sababu hii, mawasiliano miongoni mwa Wafini huchukuliwa wakati mwingine kwamba hayana nidhamu katika mitazamo ya wahamiaji.

Maombi ni nadra sana katika sehemu za kazi nchini Ufini. Kwa Wafini masuala ya dini na mambo ya mtu binafsi ambayo hayafai kuletwa kazini. Baadhi ya sehemu za kazi zimetenga sehemu ya kusali ikiwa wafanyakazi wengi wataomba sehemu ya kusali. Ikiwa mfanyakazi anahitaji muda wa kusali muda wa kazi, ni lazima asali wakati wa mapumziko. Ishara wazi za dini kama vile hijabu zinaruhusiwa nchini Ufini, lakini mavazi rasmi ya kazini unayopewa kwa mfano kwa sababu ya usalama lazima uyavae. Haya ni masuala ambayo unaweza kujadiliana na kukubaliana na mwajiri wako.

Pakua hapa yaliyomo katika kurasa huu katika muundo wa PDF.